Tuesday, July 19, 2016

IJUE DINI YA KIISLAM


Swali: "Uislamu ni nini ?
Neno Uislam limetokana na neno Islam ambalo kiini chake ni (SLM) au Salam, ambayo maana yake ni amani au kujisalimisha. Kwa hiyo kimaana, neno Uislamu (Islam) ni kule kupatikana amani ya ndani na nje kunakotokana na kujisalimisha kwa Muumba (s.w.). Kwa maana nyingine Uislamu ni kufuata mwenendo mwema unaozingatia maelekezo ya Muumba au kwa maana ingine

"Uislamu" maana yake "anayetii Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mungu wa pekee wa kweli na kwamba Muhammad alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur'an ni kitabu takatifu cha Uislamu.




NGUZO KUU ZA UISLAM
Imani ya dini ya Uislam una nguzo kuu tano, nazo ni:-

1. Shahada: "Hapana Mola ( Mwenyezi Mungu ) apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa  ALLAH na Muhammad ( S.A.W )  ni Mtume  wa Mungu." 




2. Swala:. Kuswali swala tano Alfajiri ( saa kumi na moja Alfajiri ) ,Adhuhuri ( saa saba mchana ), Alasiri ( saa Kumi jioni ) , Magharibi ( saa kumi na mbili jioni )  na Insha ( saa mbili usiku )






3. Kutoa Zaka: mtu lazima atoe kwa ajili ya masikini, asilimia fulani ya pato lake kulingana na anavyopata Mali zake kwa mwaka  vile wote hutoka kwa Mwenyezi Mungu. 






4. kufunga Ramadhani: kando ya kufunga mara kwa mara, Waislamu wote lazima wafunge wakati wa  Mwezi Mtukufu wa  Ramadhani (mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu), siku ishirini na tisa  (29) kama mwezi ukiindama na kama haujaandama ni lazima kumalizia siku thelathini (30).




5. Hija: Kwenda kuhiji  Makka kwa mwenye uwezo (Makkah) angalau mara moja katika maisha ya mtu (wakati wa mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya Kiislamu). 



NGUZO KUU ZA IMANI
Uislam una nguzo sita za Imani, nazo ni:-
1. Kumuamini ALLAH ( Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote )
2. Kuamini Malaika wa ALLAH 
3. Kuviamini vitabu Takatifu vya ALLAH Qurani, Injili na Torati 




4. Kuamini Mitume wote wa ALLAH
5. Kuamini siku ya mwisho ( Kiama) 
6. Kuamini Qadari ya ALLAH ( ya kheri au ya shari ) kuwa inatoka kwa ALLAH 




NA NGUZO YA TATU NA YA MWISHO NI IHSANI.

Na Nguzo yake ni Moja nayo ni:-
1.Kumuabudu Allah kama unamuona Kama humuoni yeye anakuona wewe.




Huu kwa muhtasari ndio Uislamu, dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha kwa wanadamu wote waliochaguliwa na Allah Mola Muumba wao: |………LEO NIMEKUKAMILISHENI DINI YENU NA KUKUTIMIZIENI NEEMA YANGU NA NIMEKUPENDELEENI UISLAMU UWE DINI YENU ………….” (5:3) elewa na ufahamu kwamba kuishi nje ya dini hii ni kulikana umbile lako kwani UISLAMU NI HAKI YAKO YA KUZALIWA uliyopewa hadiya (zawadi) na Mola Muumba wako.

KUTOA ZAKA

KUTOA ZAKA

PAMOJA na kuwa zaka ni miongoni mwa nguzo tano za Kiislamu, lakini pia ni kiungo muhimu kati ya tabaka la matajiri na masikini, kwani utekelezaji wa nguzo hii unaleta ufanisi katika kuziba mwanya uliojitokeza kati ya matabaka mawili haya. Somo hili litasaidia kuwaelimisha Waislamu umuhimu wa zaka na jinsi ya kutekeleza nguzo hii muhimu.

Nini maana ya zaka:
Zaka maana yake ni baraka, utakaso, ziada na wema, mambo ambayo upatikanaji kwa kukusanywa viwango maalumu vya mali kutoka kwa wenye uwezo na kupewa watu wasiojiweza au wanaohitaji. Tofauti kubwa iliyopo kati ya zaka na sadaka ni kuwa, zaka ni tendo la lazima ambapo sadaka ni tendo la hiari (hisani).

Hukumu ya kutoa zaka:
Kutoa zaka ni jambo la lazima kwa Muislamu mwenye uwezo uliotajwa na sheria ya Kiislamu, Muislamu huyo akiacha kutoa zaka huwa ni mkosa anayestahili kuadhibiwa mbele ya Mungu.

Mali ipasayo kutolewa zaka: 
Kitu chochote kile kinachomilikiwa na kutumika kwa maslahi ya binadamu ni mali ipasayo kutolewa zaka, hata hivyo, kuna mambo maalum yanayozingatiwa katika mali hiyo kama vile uzalishaji, kufikia lengo maalum na kupitiwa na muda wa mwaka.

Aina za zaka: 
Kuna aina nyingi za zaka, zifuatazo ni baadhi ya aina hizo:
Zaka ya Akiba, mali yoyote iliyowekwa kama akiba mahali popote pale kwa lengo la kuihifadhi hutolewa zaka. Utaratibu wa zaka hii huwa kama ifuatavyo:
Iwe na thamani isiyopungua thamani ya gramu 85 za dhahabu safi (525,000/= Tsh).
Kinachotolewa ni asilimia 2.5 ya mali yote.
Iwe ina umri wa mwaka mmoja tokea imewekwa au kutolewa zaka.

Zaka ya mifugo 




 Muislamu anayemiliki ng’ombe 30 anapaswa kutoa ng’ombe mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja, na yule anayemiliki ng’ombe 40 atoe ng’ombe mwenye umri wa miaka miwili, utaratibu huu utumike katika kila kundi la ng’ombe 30 na ng’ombe 40, pia inaruhusika kutoa thamani ya ng’ombe waliotajwa. Kuhusu mbuzi na kondoo atatoa katika kila mbuzi au kondoo 100 mnyama mmoja anayehusika au thamani yake. Jambo muhimu ni kuzingatia muda wa mwaka moja tokea kunzishwa kwa ufugaji au kutolewa kwa zaka. 

Zaka ya mavuno



Kila kinachovunwa kutoka ardhini au baharini kinapaswa kutolewa zaka mradi tu mavuno hayo yana uzito usiopungua kilo 653 (gunia sita na nusu), kinachotolewa ni kilo 65.3 iwapo kilimo hakikutegemea gharama za kitaalamu, vinginevyo mkulima atapaswa kutoa kilo 33 tu kwa kila kilo 653 anazozivuna. 


Zaka ya biashara


Mali yoyote iliyotengezwa kwa ajili ya uzalishaji inapaswa kutolewa zaka mradi tu ina thamani isiyopungua shilingi 525,000 za Kitanzania. Kinachotolewa ni asilimia 20% (1/5) ya faida iliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja. 

Zaka ya machimbo 


Kila kinachochimbwa ardhini au kukusanywa kutoka baharini miongoni mwa madini kinapaswa kutolewa zaka, kinachotolewa ni asilimia 20% ya thamani ya madini yaliyochimbwa au kukusanywa. 




Wanaostahiki kupewa zaka: 
Qur’an tukufu imetaja jamii nane za watu wanaostahiki kupewa zaka, nao ni hawa wafuatao: 
Mafukara: Hawa ni watu ambao hawamudu kupata mahitaji yao ya lazima kila siku. 

MasikiniHawa ni watu ambao hawamudu kupata mahitaji yao ya lazima kwa uhakika. 

Wenye madeni: Mtu au kikundi cha watu wenye madeni wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili waweze kulipa madeni yao. 

Watumishi wa zaka: Watu wanaotumika kukusanya na kusambaza zaka wapewe sehemu ya zaka hiyo kwa lengo la kuwafanya wasiwe na tamaa dhidi ya mali wanayoifanyia kazi. 

Harakati za ukombozi: Mtu au kikundi cha watu kinachotaka kujikomboa kutoka utumwani au kutawaliwa kimabavu wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili kufanikisha lengo lao. 

Wanaosilimu: Watu wanaoingia katika dini ya Kiislamu wanastahiki kupewa zaka ili waweze kulingana na maisha yao mapya ya Kiislamu endapo kuna hitaji la kufanya hivyo kutokana na mwengine kutengwa na jamii yao au ndugu zao amabao walikuwa wakiwategemea. 

Wanaopatwa na maafa: Watu waliopatwa na maafa wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili waweze kufarijika dhidi ya maafa yaliyowapata. 

Wanaoendeleza dini ya Kiislamu: Kila anayeshughulika na miradi ya kuiendeleza dini ya Kiislamu kama vile kufundisha, kujenga Misikiti, shule na hospitali anastahiki kupewa zaka ili kufanikisha malengo hayo. 

Mwisho: 

Wanazuoni wengi wa Kiislamu wameelezea umuhimu wa kuwa na chombo maalum cha kukusanya na kusambaza zaka badala ya kila tajiri kujitolea zaka kwa utaratibu wake binafsi, hali hii haipendezi wala haileti ufanisi mzuri katika kuuendeleza Uislamu,imeshauriwa zaka ikusanywe kwa pamoja kisha isambazwe kwa wahusika.  

JINSI YA KUSIMAMISHA SWALA


Baada ya Kuangalia Masomo ya awali maana ya Uslam, Nguzo tano za Uislam na Nguzo sita za Iman  pamoja na kuchukuaudhu , leo tunaangalia jinsi ya kushiriki swala ya Alfajir, Adhuhur,Alasir, Magharbi na Insha .


 Kwanza Kabisa picha hapo juu inaelekeza hatua saba muhimu zinazopatikana katika swala

Hapa nimekuletea clip inayoonyesha jinsi ya kusimamisha swala pamoja na kutia nia kiufasaha